RISALA YA MAHAFALI YA NNE
YA KIDATO CHA IV 2011
KWA MGENI RASMI –
Mh MAKONGORO MAHANGA (MB), NAIBU WAZIRI- KAZI NA VIJANA
TAREHE 10/09/2011
Utangulizi:-
Ndugu Mgeni
rasmi, Mlezi wa shule ya sekondari, mkurugenzi wa shule za Paradigms, wazazi,
wageni waalikwa, waalimu, wanafunzi, mabibi na mabwana, itifaki imezingatiwa,
HABARI ZA
ASUBUHI
Awali
ya yote napenda kumshukuru Mwenyeezi Mungu ambaye kwa Mapenzi Yake Ametupa
uhai na kutuwezesha kuwepo mahali
hapa.
Aidha
napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa mgeni rasmi kwa kukubali kujumuika nasi leo katika sherehe za mahafali
ya 4 wanafunzi wetu wa kidato cha nne ,na ya 3 ya darasa la saba na darasa la awali 2011. Tunasema ahsante sana na karibu sana
Paradigms.
Ndugu
mgeni rasmi, Shule za Paradigms ni shule
zinazotoa elimu ya awali, msingi, sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha
sita, Chuo cha Ualimu ambapo tunatoa kozi za mafunzo ya ualimu wa shule za
awali, shule za msingi (GRADE III A) na stashahada ya ualimu (Diploma in Education)
pamoja na chuo cha COMPUTER ambapo tunatoa kozi za vyeti na stashada za
Tekinohama (ICT). Shule hizi zipo chini
ya kampuni ya uendelezaji elimu iitwayo Paradigms Institute Ltd.
Shule
hizi zinapokea na kusomesha wavulana na wasichana', wa kutwa na bweni na
tunatoa huduma iliyobuniwa na kuratibiwa vizuri kuwaridhisha wateja wa makundi
mbalimbali. Tunafundisha masomo kulingana na mitaala ya Taasisi ya Elimu ya
Taifa (Tanzania Institute of Education) inayosimamiwa na kutahiniwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kwa
kutumia lugha ya kiingereza isipokuwa somo la Kiswahili.
Ndugu
mgeni rasmi, kuwepo kwa shule zetu nje ya mji, ukubwa wa eneo la shule na
mchanganyiko wa shule 4, kumetengeneza mazingira murua ya kufundisha na
kujisomea.
Ndugu
mgeni rasmi, shule za Paradigms zimeanza kwa nyakati tofauti, kama
ifuatavyo:- Februari 2007, shule ya
sekondari ilianza kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha tano, Januari
2008, shule ya awali na msingi ilianzishwa kwa darasa la kwanza mpaka la Sita ,
Julai 2009, chuo cha ualimu kilianzishwa na Julai 2011, tulifungua chuo cha
COMPUTER. Shule zote hizi zimesajiliwa
na zinaendeshwa kwa taratibu sahihi zilizowekwa na Taifa na kusimamiwa na
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
TAALUMA
Ndugu
mgeni rasmi, taaluma ndilo lengo letu la msingi la kuwepo hapa. Kama
tulivyoeleza hapo juu, shule zetu zina umri wa Kati ya miezi 3 mpaka miaka 4.5.
Mzunguko wa elimu ni baina ya miaka 2 mpaka 7. Ili kuandaa na kutekeleza
mkakati unaopimika unahitajika kutumikia mizunguko 2 au zaidi. Ndio kwanza
tunamalizia mzunguko wa kwanza na hivyo tuko katika kipindi Cha tathmini ya mafanikio na changamoto za Mzunguko wa
kwanza ili tuweze kujipanga vizuri kwa kukabiliana nazo kwa mikakati sahihi.
Mifano ifuatayo inaelezea fursa na vikwazo tulivyokuwa navyo. Shule ya msingi ilianza 2008 ikiwa na
wanafunzi 8 wa darasa la kwanza. Kwa sasa wanafunzi hao wako darasa la 4. Hata
hivyo utashangaa kuwa zao letu la kwanza la darasa la Saba lilikuwa 2009, 2010
na 2011. Hii ina maana kuwa tulilazimika kupokea wanafunzi wa darasa la 6 toka
shule mbali mbali zikiwemo zile zinazotumia lugha ya Kiswahili na tukaweza
kuwaandaa kwa muda mfupi na wakafaulu. Kadhalika shule yetu ya sekondari
ilianza mwaka 2007 na ikaanza kutoa matunda ya kidato cha nne 2008, mwaka
2008,2009,2010 wakati kundi la kwanza lilitakiwa litoke 2010. Hii ina maana
kuwa tulipokea wanafunzi waliokuwa wanasoma katika shule nyingine na
tukawaandaa kwa kipindi kifupi kabla ya kufanya mitihani yao. Uzoefu tulioupata
umetupa nafasi ya kuandaa mikakati
sahihi ya kutuwezesha kusonga mbele kwa uhakika na kwa kujiamini.
Ndugu mgeni rasmi, shule za
Paradigms zimekuwa na mafanikio mbalimbali katika nyanja za kitaaluma toka
zilipoanzishwa hadi leo. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na:
Kuweza kuongeza kiwango cha
ufaulu kwa 70% kwa madarasa yote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Hilo
limejihiridhisha katika matokeo yetu ya kidato cha nne na sita ya mitihani ya
taifa kwa mwaka 2009 na 2010. Kwa mfano, matokeo ya kidato cha nne ya mwaka
jana(2010) tulifanikiwa kufuta divisheni ziro ikizingatiwa kwamba mwaka huo
wanafunzi wengi walifeli sana.Kwa kidato cha sita 90% ya watahiniwa wa mwaka
2010 wamefanikiwa kuendelea na elimu ya juu.
Ndugu mgeni rasmi,
ikumbukwe kwamba wanafunzi hawa tuliwapokea wakiwa katika hali mbaya sana
kitaaluma, lakini tulifanya juhudi kubwa kuwasaidia katika kipindi kifupi
tulichokaa nao. Matokeo ya juhudi hizo
ni ya kujivunia, kwani ni kazi iliyofanyika kwa muda mfupi sana.
Kwa mwaka huu 2011
wanafunzi 30 walihitimu kidato cha sita, wanafunzi 9 kati yao walisoma kidato
cha tano huku wanarudia mitihani ya kidato cha IV ili waweze kupata sifa za
kufanya mtihani wa kidato cha sita.
Wanafunzi hawa walifanikiwa kupata sifa hizo zilizowawezesha kufanya
mtihani wa kidato cha sita na wote walifaulu na 75% yao wamepata nafasi ya
kuendelea na elimu ya juu katika vyuo vikuu mbali mbali ndani na nje ya nchi.
Tunajivunia matokeo haya
kwani yanatokana na juhudi na kazi nzuri iliyofanywa na timu ya waalimu wetu.
Ndugu mgeni rasmi, katika
kuonyesha kweli tumejipanga katika kujiimarisha katika kutoa elimu bora,
tumefanikiwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa waalimu wetu wa ndani ili kuendana na
mabadiliko ya mitaala na kuweza kuboresha huduma zetu zaidi. Kwa mfano; mwanzoni
mwa mwaka huu tulitoa mafunzo ya jinsi ya kumuhudumia mteja tukiamini kwamba
mteja ndio shina la kufanikinikisha adhima na lengo la serikali na taasisi yetu
katika utoaji elimu bora.
Pia kutokana na mabadiliko ya mitaala mara kwa
mara tumefanikiwa kuwaendeleza waalimu kupitia mafunzo mbalimbali ya kujifunza
na ufundishaji ambayo ni mafunzo elekezi ya jinsi ya kutunga mitihani kuendana
na mtaala mpya, kusaisha mitihani pamoja na mbinu mpya zinazomshirikisha
mwanafunzi katika kujifunza kama inavyoelekezwa katika mtaala mpya.
Ndugu mgeni rasmi, mwaka
huu tunao wanafunzi 48 wanaohitimu kidato cha nne, 17 darasa la saba. Asilimia 75 kati ya wanafunzi hao walihamia
shuleni kwetu katika vidato na madarasa mbali mbali. Kadhalika tunao wanafunzi 14 wanaomaliza shule
ya awali. Hawa wote tumewaandaa, tumewapima na tunaimani kuwa zao la mwaka huu
litakuwa bora zaidi ya lile la mwaka jana.
Ndugu mgeni rasmi, katika
ngazi ya shule ya msingi, tumekuwa na mafanikio makubwa sana katika kuhakikisha
tunafikia kilele cha mafanikio. Kwa mfano maendeleo ya kitaaluma yamekuwa
yakipanda mwaka hadi mwaka kuanzia 2009 hadi sasa. Kipimo cha ukuaji huu wa
kitaaluma umepimwa kulinganisha na shule nyingine katika ngazi ya wilaya,mkoa
na kitaifa. Kwa mfano zifuatazo ni takwimu zinazoonyesha kiwango cha kukua kwa
ufaulu wetu katika shule ya msingi;
Mwaka 2009-shule yetu ya msingi ilikuwa
nafasi ya 31 kiwilaya kati ya shule 74, nafasi ya 185 kimkoa kati ya shule 407,
na kitaifa nafasi ya 2205 kati ya 14376 wakat Mwaka 2010, shule yetu ilikuwa ya 19 kiwilaya kati
ya shule 82, kimkoa shule ilikuwa nafasi ya 60 kati ya shule 433 na kitaifa
shule ilkuwa nafasi ya 646 kati ya 14759.
Ndugu mgeni rasmi, kutokana
na data hizo inaonyesha ni jinsi gani maendeleo ya shule yetu yamekuwa yakikua
kila mwaka. Na kwa mwaka huu tunategemea kupanda zaidi katika kiwango cha
kufaulisha na kufikia kiwango cha juu zaidi kitaifa. Mkakati wetu ni kuwa 10
bora kiwilaya kabla ya 2013 na 10
Bora kitaifa ifikapo 2015.
Tumedhamiria, tumejipanga, tumefanya mabadiliko
makubwa ya kiutendaji na kiusimamizi na tuna imani kuwa tutashinda
Mkakati wetu ni kuendelea
kuboresha huduma zetu kitaaluma na kinidhamu mpaka tutakapokuwa mfano bora wa
kuigwa – a model school – yaani Paradigm.
Njia tupitayo ni nyembamba na ngumu, hata hivyo dhamira yetu ni kubwa na
tunaamini kuwa hakuna kitakachotuzuia.
Ndugu
mgeni rasmi, katika kuboresha taaluma wanafunzi wetu wa shule zote nne wana
nafasi ya kusoma somo la kompyuta ambapo kwa kufahamu matumizi ya kompyuta ni
rahisi kwa wao (wanafunzi) kuweza kutumia kompyuta katika zoezi zima la
kufundishwa na kujifunza. Tunayo maabara ya kisasa ya tekinohama (ICT)
iliyounganishwa na mfumo huru wa mtandao (wireless internet connection) kiasi
cha kumwezesha kila mwanafunzi kuwasiliana na ulimwengu kupitia njia ya mtandao
kwa urahisi zaidi.Tumelazimika kusisitiza na kuhimiza somo hili kwa kutambua
ukweli kuwa maisha yetu sasa yanategemea tekinohama.
Ndugu
mgeni rasmi, kukua kwetu kitaaluma kumejengwa na kuwezeshwa na dhamira ya
wakurugenzi, bodi ya shule na wadau mbali mbali kwa kutuwezesha kupata
rasilimali sahihi za kuendeshea shule zikiwemo; madarasa, maabara, maktaba,
vifaa na kemikali vinavyokidhi haja ya sasa na wakati ujao.
Ndugu
mgeni rasmi, Pamoja na kwamba kuna mambo mengi yanayochangia matokeo ya Taaluma
kuwa mazuri au mabaya; ufundishaji, usimamizi na ufuatiliaji wa karibu ni
mkakati sahihi unaopaswa kuratibiwa na kuhakikiwa kwa umakini mkubwa. Ili
kufikia lengo hilo, tumelazimika kuwa na mikakati mingi na endelevu. Sehemu ya
mikakati hiyo ni; kuwapima wanafunzi wanapojiunga nasi kujua uwezo wao,
kuwapima kila mwezi kujua tija ya utendaji wetu na juhudi zao, kuwachuja kila
mwaka kabla hawajajiunga na kidato kinachofuata. Tumeandaa utaratibu maalum wa
kuwafuatilia kwa ukaribu waalimu wetu kuona kama wanafundisha kwa umahiri na
ukamilifu. Ili kujihakikishia kuwa hatufanyi makosa, tumenunua na kufunga
kamera, CCTV CAMERAS madarsani na SERVER yenye uwezo wa kuhifadhi matukio yetu
kwa siku 90. Utaratibu huu umekuza ari ya utendaji, na tayari waalimu 4
waliokwazwa na utaratibu huu wameshakimbia kazi. Tunawaomba wateja wetu
watuelewe, washirikiane nasi na watuvumilie.
NIDHAMU
Ndugu
mgeni rasmi, nina imani kabisa kuwa wewe utakuwa shahidi yangu mbele ya umati
huu wa wazazi pamoja na wanafunzi ya kwamba “Hakuna Elimu bila Nidhamu”.
Changamoto
za nidhamu kwa wanafunzi zinakuwa siku hadi siku, wanafunzi wanadai demokrasia
na uhuru zaidi. Wazazi wanadai malezi na
kusikiliza zaidi (mteja ni mfalme) na sisi tumedhamiria kuwa kituo cha malezi
bora na elimu iliyotukuka.
Ndugu
mgeni rasmi, changamoto iliyopo ni tafsiri ya haki na wajibu baina ya waalimu,
wazazi, wanafunzi na jamii. Mkanganyiko
huu wa tafsiri ukienda sambamba na umri wa vijana wetu na athari za dunia kuwa
kijiji (globalization) vimekuwa vikwazo vikubwa sana katika kufikia malengo
yetu ya kukuza nidhamu. Taasisi
imejipanga na imechukua hatua mahsusi kuona kuwa tunajenga familia yenye
nidhamu na inayofuata maadili na miiko ya Taifa letu.
Ndugu
mgeni rasmi, tunaomba wizara, wazazi, jamii na taifa kwa ujumla tujipange upya
kuangalia mihimili ya utamaduni wetu, na kutafuta mbinu muafaka za kuwekeza
katika nidhamu za watoto wetu.
Tukijipanga vizuri na kushirikiana shule zitabaki kuwa vituo vikuu vya
malezi na utamaduni wa Taifa letu.
Ndugu
mgeni rasmi, katika kupambana na changamoto hizi tumefanikiwa kuunda kamati ya
nidhamu pamoja na ushauri nasaha ambapo imekuwa na kazi ngumu ya kuwarudi
wanafunzi ili wafuate maadili na tamaduni zetu.
Pia
tunakutana na wazazi wa wanafunzi wanaoonyesha kiwango kikubwa cha utovu wa
nidhamu na kujadili kwa pamoja makosa aliyotenda mwanae (mwanafunzi). Tumeunda kamati ya wazazi ya ushauri ili
kuhakikisha utawala bora na uwazi katika utekelezaji wa majukumu yetu.
MOTISHA
Kumiliki
na kuendesha shule ni changamoto inayohitaji kuangaliwa kutumia tundu la 3 (the
third dimension) na kwa umakini mkubwa. Lazima kutambua kuwa kuna wadau zaidi
ya 8 wenye maslahi na shule. Kinachotatiza zaidi ni kuwa, sio tu kuwa wana
maslahi na shule, bali pia wana maslahi yao binafsi yanayokinzana na yale ya
shule. Kazi kubwa tuliyonayo ni namna ya kutambua maslahi yao na kujipanga
kuyakidhi bila kuathiri yale ya taasisi.
Tumejipanga
na tunatoa motisha zifuatazo kwa wadau wetu.
►nyumba
kwa waalimu; waalimu 10 kati ya 25 wanaishi katika nyumba za shule.
►mikopo
midogo midogo; wafanyakazi wanakopeshwa
mishahara 2 kukidhi
mahitaji yao tunapokuwa na uwezo.
►ajira;
wanafunzi wetu wanaomaliza na kufaulu vizuri wanaajiriwa na taasisi
yetu
►masomo
kazini; waalimu wanaofanya kazi zao vizuri hupata fursa ya
kuendelezwa katika ngazi inayofuata.
►wanafunzi
wanaofaulu vizuri hupongezwa kwa njia mbali mbali ikiwa ni pamoja
na safari za kutembelea maeneo ya
kihistoria.
►
waalimu wanaoshindwa kutimiza wajibu wao vizuri huachishwa kazi
►
wanafunzi wasiokuwa na nidhamu huachishwa shule
CHANGAMOTO
Shule
zetu zinakabiliwa na changamoto kadhaa zinazokwaza ufanisi. Baadhi yake ni hizi zifuatazo:-
A. CHANGAMOTO ZA
KITAASISI
1. MAJI
Shule
zetu zinavyo visima 3 vinavyotoa maji ardhini ya kutosheleza shule. Hata hivyo maji haya yana chumvi. Upatikanaji wa maji yasiyokuwa na chumvi na
ya kutosheleza, ni ama kutegemea Dawasa / Dawasco au kuvuna maji ya mvua au
vyote kwa pamoja, Kunahitajika kujengwa matanki yenye ujazo usiopungua gallon
250 m kwa ajili ya kutosheleza matumizi ya sasa na baadae angalau kwa siku
100.Mradi huu unahitaji uwekezaji wa Tshs 86 m.
2 . UMEME
Ndugu mgeni rasmi, tatizo la umeme limekuwa ni
kikwazo kikubwa katika kufikia lengo la kutoa huduma na kuipata huduma hiyo kwa
ujumla. Hii ni changamoto kwa maana kwamba utoaji wa elimu katika shule yetu
unategemea zaidi kujifunza na kufundisha kwa kutumia vifaa vingi vinavyotumia
umeme kwa mfano, matumizi projector kufundishia, kuwashia kamera za usimamizi,
kufundishia computer na huduma za masomo
kupitia mtandao, mwanga kwa ajili ya kujisomea usiku, Tunaomba utufikishie
kilio chetu serikalini ili kama ni lazima kufanya mgawo waangalie maeneo ya
shule Kama inavyofanyika katika kambi za jeshi na chuo kikuu cha Dar Es Salaam.
3. MICHEZO
Pamoja
na kuwa tunavyo viwanja / maeneo ya michezo makubwa kuliko shule yeyote katika
wilaya yetu , tunapaswa kuwekeza kikamilifu katika ujenzi na kuendeleza viwanja
hivi pamoja na vifaa ili kuboresha na kuendeleza michezo hapa shuleni. Ni imani
yetu kuwa wizara yako itatusaidia kupata mfadhili au mbinu za kuwekeza katika
eneo hili la michezo.
B.CHANGAMOTO ZA
JUMLA
Ndugu
mgeni rasmi, pamoja na mafanikio tuliyoeleza juu, bado taasisi yetu, na
nyingine zinazotoa elimu nchini, tunakabiliwa na changamoto nyingi. Baadhi yake ni hizi zifuatazo.
(a) Riba:-
Uwekezaji
katika elimu unahitaji mtaji mkubwa
sana; Sisi kwa mfano tumeshawekeza zaidi ya bilioni moja, 50% ikiwa ni
mikopo toka benki mbalimbali na tumeomba zaidi ya sh. 1.3 bilioni kwa ajili ya
kuboresha huduma zetu mwakani.
Tunategemea kuwekeza bilioni 10 ifikapo mwaka 2017; Fedha zote hizi
zinatozwa riba ya 20% - 24% kwa mwaka.
Ni
ukweli usiofichika kwamba haiwezekani kuboresha elimu nchini kwa riba za namna
hii. Tunaomba na tunashauri serikali ianzishe mfuko au benki maalumu ya
uwekezaji katika huduma ya elimu itakayotoza riba isiyozidi 5%; Katika hili
ifahamike kuwa riba isipopungua hatimaye mteja ndiye atakayelipia riba na matokeo
yake ada zitaendelea kupanda na Watanzania wengi watakosa nafasi za masomo
kwani si rahisi serikali iweze kumudu kutoa huduma hii peke yake.
(b) Kodi
za majengo:
Ndugu
mgeni rasmi, kazi ya kujenga na kuendesha shule za msingi na sekondari ni halmashauri
za mji, manispaa na jiji. Halmashauri hizi hupaswa kutoza kodi
Mbali toka kwa wakazi wake ili ziweze kutimiza jukumu hili. Wale
waliotozwa kodi walipaswa kupatiwa haki ya
elimu watoto wao kutokana na kodi hizo. Bahati mbaya Halmashauri hizo zimeshindwa kujenga
shule za kutosha kusomesha watoto hawa.
Ni kwa misingi hiyo ndio maana
taasisi na watu binafsi wameamua kujenga shule za binafsi kuzisaidia
Halmashauri kutimiza wajibu wao. Kama
halmashauri zitaendelea kutoza kodi hizi (mfano property tax) na serikali kuu ikiendelea kutoza ( income
tax ) ni kuwatoza wananchi wake kodi
mara mbili kwani hatimaye kodi hizo zitaingizwa kwenye ada, hivyo tunapendekeza
kuwa shule zote zisitozwe kodi ya majengo wala ya mapato ili ziwe na uwezo wa
kuboresha huduma na kuzitoa kwa gharama nafuu.
(c) Sheria
na kanuni za elimu:
Ndugu
mgeni rasmi, sheria na kanuni zinazosimamia elimu ni kali sana na yawezekana
dhamira yake ni njema kwa manufaa ya Taifa letu tukufu la Tanzania. Hata hivyo kwa namna zilivyo zinakwaza na
kuchelewesha walengwa kufikia malengo yao kielimu. Tunadhani tunachopaswa kufanya ni kuandaa
kipimo muafaka cha uelewa mwishoni mwa mafunzo. Katika hili, tunapendekeza
kanuni zifuatazo ziangaliwe upya.
(i) Kanuni
ya kumlazimisha mwanafunzi awe na alama (3 credits) kabla ya kujiunga na kidato
cha (V) tano, ibadilishwe na badala yake atakiwe kuwa nazo kabla hajaruhusiwa
kufanya mtihani, wa kidato cha sita (VI).
Kanuni
inayoelekeza kumlazimisha mwanafunzi anayetaka kujiunga na chuo cha ualimu awe
amemaliza shule si zaidi ya miaka mitano nyuma ibadilishwe na badala yake iwe
mwaka wowote ili kumpa nafasi kila Mtanzania mwenye sifa ya kusomea ualimu
asome. Hii italiwezesha Taifa kupata
idadi kubwa ya waalimu ili kukidhi haja ya mahitaji makubwa yaliyopo. Changamoto za vyeti vya miaka ya nyuma
zitafutiwe namna ya kitaalam ya kukabiliana nazo.
Kurudia
darasa. Lazima tufanye maamuzi magumu katika masuala nyeti. Inatupasa kuamua
kama shule ni taasisi za makuzi au elimu. Inatupasa kuamua kama kipimo cha
elimu kinapaswa kufanywa mwishoni au muda wote. Tunapaswa kuamua ikiwa ni
busara kuendelea mbele na mwanafunzi mwenye uwezo mdogo hata kama tunajua kuwa hatimaye hatafaulu ama
tumsubirishe mpaka aive. Hivi tunapomlazimiza mwanafunzi ambaye mlezi wake yuko
tayari kumlipia Ada ya kurudia tunafanya hivyo kwa maslahi ya nani? Inashauriwa
kuwa tufufue utaratibu wa kuwapima wanafunzi kila mwaka, wale wasiofikia
viwango walazimishwe kurudia mwaka, hasa kama wadhamini wao watakubali
kuwalipia ada ya kurudia.
Mabadiliko
ya mitaala. Ubadilishaji wa mitaala ni jambo jema likifanywa kwa umakini. Kwa
bahati mbaya sana, ubadilishaji wa mitaala yetu umekuwa ukifanywa bila
maandalizi ya kutosha na hivyo kuwachanganya wadau na kutokuleta tija
inayokusudiwa. Tunaomba wale wanaoamua kubadilisha mitaala watambue kuwa
kunahitajika uwekezaji mkubwa katika mafunzo kwa waalimu na wakufunzi. Lazima
uwekezaji huu ufanywe wakati muafaka na kwa maslahi ya wadau wote.
Taarifa
za maeneleo ya mwanafunzi kitaaluma. Kuna tetesi kuwa kumekuwa na mkanaganyiko mkubwa wa
uandaaji wa taarifa hizi kiasi cha kuwafanya watumiaji ama kuhoji uhalali wake
na hata kuamua kutozitumia kabisa. Kama tetesi hizi zina ukweli, yatupasa
kuliangalia kwa makini kwa kuwa, hatuwezi kuharibu mizani na tukaendelea
kujidai kuwa sie ni wapimaji wazuri. Mizania mbovu lazima itoe majibu mabovu.
Upungufu
wa waalimu wa III A na Diploma: Ndugu mgeni rasmi, inakisiwa kuwa wastani wa
waalimu dhidi ya wanafunzi katika shule za sekonari 1:75 wakati ile wa shule za msingi unakaribia
1:85. Kwa sasa serikali ina uwezo wa kusomesha 2% kwa mwaka. Kwa utaratibu huu
tutafikia lengo la 1:40 miaka 50 ijayo. Kama serikali ikiamua kuwalipia AMA
kuwakopesha wanaosomea Daraja la IIIA na Diploma, sekta binafsi inaweza
kuzalisha waalimu 500, 000 kwa mwaka na kulimaliza tatizo la waalimu ndani ya
miaka 5 ijayo. Tunashauri yafanyike maamuzi magumu.
HITIMISHO:
Ndugu
mgeni rasmi, tunakufahamu wewe, marafiki zako na uwezo wako. Tunaifahamu nafasi yako katika jamii na
heshima uliyojijengea katika kuhudumia watu.
Ni imani yetu kuwa, utapata fursa ya kuipitia risala hii kwa umakini na
kushirikiana nasi kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazotukabili.
Nashukuru
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment